Sekretarieti ya Ajira yatoa elimu kwa Wahitimu wa Chuo cha Kodi kuhusu masuala ya Ajira Serikalini.
November 17, 2017
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imefanya ziara ya kikazi katika Chuo cha Kodi kilichopo Mikocheni Jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua endelevu ya utekelezaji wa mkakati wake wa kutatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wakati wa utekelezaji wa mchakato wa Ajira Serikalini kwa kukutana na wadau wake ikiwemo wanafunzi wa vyuo mbalimbali.
Katika ziara hiyo mada mbalimbali zilitolewa kwa Wahitimu hao ikiwemo taratibu za uendeshaji wa Mchakato wa Ajira katika Utumishi wa Umma, Masharti ya msingi ya kuzingatiwa kabla na baada ya kuwasilisha maombi ya kazi, Matumizi ya TEHAMA hususani namna ya kujisajili katika mfumo wa maombi ya kazi (Recruitment Portal).
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira Bibi Riziki Abraham akiongea na wahitimu wa chuo hicho alibainisha kuwa mada hizo zimelenga kutatua changamoto pamoja na kutoa uelewa kwa wanafunzi wa Vyuo hasa wahitimu ili waweze kujua majukumu ya Sekretarieti ya Ajira, taratibu za kufuata kabla ya kuomba ajira Serikalini, namna ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili pamoja na utaratibu wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao ujulikanao kama Recruitment portal.
“Ningependa mfahamu kuwa nyie ni kati ya wadau wetu wakubwa katika kutekeleza Mchakato wa Ajira Serikalini, na tunatambua baada ya mahafali wengi wenu mmejipanga kuingia katika soko la ajira ambalo linahitaji watu wenye weledi na uelewa wa kutosha katika masuala mbalimbali” alisisitiza Riziki.
Riziki aliongeza kuwa, Sekretarieti ya Ajira katika kukabiliana na changamoto inazokumbana nazo wakati wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira imeamua kuwa na mkakati wa kuwafuata wadau wake kuzungumza ili kuwaelimisha na kupata mrejesho kutoka kwao ili wanapoanza kuwasilisha maombi ya kazi tayari wawe na uelewa na kufahamu vyema taratibu za kuomba kazi, namna ya kuandaa wasifu binafsi (CV) namna ya kuandika barua za maombi ya kazi, jinsi ya kujiandaa kabla na wakati wa usaili na utaratibu mpya wa utumaji na upokeaji wa maombi ya kazi kwa njia ya Mtandao ujulikanao kama Recruitment portal” ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kushindana katika soko la ajira nchini.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo hicho anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Dr. Lewis J Ishemoi amewashauri wanafunzi wa Chuo hicho kutambua kwamba soko la Ajira lina ushindani mkubwa kutokana na kuwa na wahitimu wengi hivyo ni lazima wajiandae kisaikolojia kushindana katika soko hilo hasa katika sekta ya Kodi ambapo Serikali inategemea wataalam kutoka chuo hicho.
Ziara hiyo ni sehemu ya muendelezo wa mkakati Sekretarieti kutembelea wadau wake ikiwemo Waajiri na Wanafunzi wa Vyuo mbalimbali nchini ili kuweza kuwajengea uwezo katika yame maeneo ambayo imekuwa ikiona kuna mapungufu badala ya kuendelea kubaki maofisini na kuwa sehemu ya kulalamikia wasioelewa. Mpaka sasa wameshakutana na wadau mbalimbali kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Welcome Back Nimam News
Blogger Comment
Facebook Comment